Matthew 21:33-46

Mfano Wa Wapangaji Waovu

(Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)

33 a “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri kwenda nchi nyingine. 34 bWakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.

35 c “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. 36 dKisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. 37Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

38 e “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ 39 fHivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.

40 “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”

41 gWakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”

42 hYesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:

“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni la ajabu machoni petu’?
43 i “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. 44 jYeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

45Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46 kWakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.

Copyright information for SwhNEN